Kiswahili Form Two Necta Format – Form Two National Assessment (FTNA).
KISWAHILI
1.0 UTANGULIZI
Fomati hii imeandaliwa ili kukidhi utunzi wa maswali ya Upimaji wa Kidato cha Pili. Fomati imezingatia muhtasari wa mwaka 2005 uliorekebishwa mwaka 2010 kwa Kidato cha Kwanza na cha Pili. Mada zote zilizomo ndani ya muhtasari wa somo la Kiswahili kwa Shule za Sekondari kwa Kidato cha Kwanza na cha Pili zimezingatiwa kikamilifu.
2.0 MALENGO YA JUMLA
Malengo ya upimaji yatahusu uwezo wa mwanafunzi katika:
2.1 Kuelewa, kutathmini na kutumia kazi za fasihi katika maisha.
2.2 Kusoma na kuelewa maandiko na vitabu mbalimbali vya Kiswahili vyenye taarifa fupi na rahisi ili kupata ujumbe mahsusi.
2.3 Kubainisha matumizi ya Kiswahili katika miktadha mbalimbali.
2.4 Kujieleza kwa Kiswahili kwa kusimulia au kuandika habari fupi kwa kuzingatia taratibu za uandishi.
2.5 Kukusanya, kubainisha, kuhakiki, kutunga na kuhifadhi kazi za fasihi simulizi kwa Kiswahili.
2.6 Kubaini matumizi sahihi ya maneno katika tungo mbalimbali za Kiswahili.
3.0 UJUZI WA JUMLA
Upimaji kwa kutumia muhtasari utazingatia ujuzi na utendaji wa mwanafunzi katika:
3.1 Kusikiliza na kuwasiliana kwa Kiswahili sanifu katika miktadha mbalimbali.
3.2 Kusoma maandiko mbalimbali ya Kiswahili kwa ufanisi.
3.3 Kuandika habari fupi kwa Kiswahili sanifu.
3.4 Kubainisha, kuhakiki na kutunga kazi za fasihi simulizi kwa Kiswahili.
3.5 Kuwasiliana kwa kutumia lugha ya ishara na alama (kwa viziwi).
3.6 Kusoma na kuandika lugha ya Kiswahili kwa kutumia herufi za breili kwa wasioona.
4.0 MUUNDO WA UPIMAJI
Kutakuwa na karatasi moja yenye sehemu A, B, C, D na E. Muda wa upimaji utakuwa saa 2:30. Jumla ya maswali yatakuwa kumi (10) na mwanafunzi atatakiwa kujibu maswali yote kwa kuzingatia maelekezo ya kila sehemu.
4.1 Sehemu A itahusu Ufahamu na itakuwa na maswali mawili (02) kuhusu kifungu cha habari. Swali la kwanza litakuwa na vipengele vinne (04). Swali la pili litahusu ufupisho. Sehemu hii itakuwa na alama kumi na tano (15).
4.2 Sehemu B itahusu Sarufi na itakuwa na maswali mawili (02) yenye vipengele vyenye kuhitaji majibu mafupi. Mwanafunzi atatakiwa kujibu maswali yote. Sehemu hii itakuwa na jumla ya alama ishirini (20).
4.3 Sehemu C itahusu Mawasiliano na Utumizi wa Lugha. Sehemu hii itakuwa na maswali mawili (02) yenye kuhitaji majibu mafupi. Mwanafunzi atatakiwa kujibu maswali yote. Sehemu hii itakuwa na jumla ya alama ishirini (20).
4.4 Sehemu D itahusu Fasihi na itajikita katika Fasihi kwa Ujumla, Uhakiki, Uhifadhi na Utunzi wa Kazi za Fasihi Simulizi. Sehemu hii itakuwa na maswali matatu (03) yenye kuhitaji majibu mafupi. Mwanafunzi atatakiwa kujibu maswali yote. Sehemu hii itakuwa na alama thelathini (30).
4.5 Sehemu E itahusu Uandishi/Utungaji na itakuwa na swali moja (01). Sehemu hii itakuwa na alama kumi na tano (15).
5.0 MADA ZITAKAZOPIMWA
Mada zifuatazo zitapimwa:
5.1 Ufahamu
5.2 Sarufi
5.3 Mawasiliano na Utumizi wa Lugha
5.4 Fasihi
5.5 Uandishi/Utungaji